Mchezaji wa DR Congo anusurika Brussels

Mbokani Haki miliki ya picha UNIAN
Image caption Mbokani akiwa uwanjani awali

Mshambuliaji mmoja wa klabu ya Norwich ya Uingereza amenusurika kwenye shambulio lililotekelezwa katika uwanja wa ndege wa Brussels.

Dieumerci Mbokani alinusurika “bila majeraha” lakini ametetemeshwa sana na shambulio hilo.

Mbokani, 30, alikuwa kwenye uwanja huo wa ndege milipuko miwili ilipotokea lakini klabu ya Norwich inasema mchezaji huyo anayetoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo sasa yuko nyumbani salama.

Watu 31 waliuawa kwenye mashambulio yaliyotekelezwa katika uwanja wa ndege na kituo cha treni mjini Brussels.

Timu ya taifa ya Ubelgiji imefutilia mbali kipindi cha mazoezi kwa heshima ya waliofariki.

Wanapangiwa kucheza dhidi ya Ureno mechi ya kirafiki uwanja wa Mfalme Baudouin mjini Brussels tarehe 29 Machi lakini sasa kuna shaka kuhusu hatima ya mechi hiyo.

Ubelgiji wamefuzu kwa fainali za Euro 2016 zitakazochezewa Ufaransa na wamo kundi E na Italia, Ireland na Sweden.