Wapiganaji 70 wa al-Shabab wauawa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Puntland ' Tumewaua Al Shabab 70'

Maafisa wa serikali ya Puntland katika jimbo la Kaskazini Mashariki mwa Somalia wanasema wamewauwa zaidi ya wapiganaji 70 wa kundi la kiislamu la Al shabab katika harakati zao dhidi ya kundi hilo la kiislam zilizoanza tangu wiki iliyopita .

Jeshi la Somalia lilivamia maeneo kadhaa katika eneo hilo mapema wiki iliyopita .

Maafisa waliwaweka mbele ya hadhara zaidi ya wafungwa 30 wakiwemo watoto ambao walisema walipewa mafunzo ya kivita na kundi hilo la Al shaabab .

Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha watoto walio kati ya umri wa miaka 12-16 wakiwa wamevalia kile kilichoonekana kama magwanda ya kijeshi.

Walikua miongoni mwa wafungwa 30 waliokamatwa kufuatia siku kadhaa za makabiliano katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo .

Baadhi ya watoto hao walizungumza na vyombo vya habari vya Somalia wakisema kuwa walilazimishwa kujiunga na kundi hilo.

Baadhi walisema waliambiwa kuwa ikiwa wangejiunga nao wakafaifika kwa kupelekwa shuleni.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maafisa waliwaweka mbele ya hadhara zaidi ya wafungwa 30 wakiwemo watoto ambao walisema walipewa mafunzo ya kivita na kundi hilo la Al shaabab .

Haijawa wazi mpango wa maafisa hao kuhusiana na watoto hao, lakini kamanda wa kijeshi katika mojawapo ya maeneo ambako mapigano hayo yalifanyika ameiambia BBC kwamba watakabiliwa na mkono wa sheria.

''Ni maadui wa jimbo letu, Ni maadau wa Somalia na dunia nzima,'' amesema.

''Kwa hiyo tutafuata sheria.Tutawapeleka mahakamani na ni jukumu la mahakama kuamua ni vipi watashughulikiwa '' alisema afisa huyo wa ngazi ya juu.

''Hii imekua ni ishara tosha ya kwamba makundi ya wapiganaji yamekua yakiwatumia watoto katika harakati za kivita.'' aliongezea kusema.

Mashambulio ya hivi karibuni yamezusha hofu katika sehemu hiyo ya Somalia iliyokua na amani kwa kipindi cha miaka 25.

Sasa kuna hofu kuwa huenda vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Somalia vitaendelea.