Afisa mwingine wa jeshi auawa Burundi

Haki miliki ya picha
Image caption Afisa mwingine wa jeshi auawa Burundi

Afisa mwengine wa ngazi ya juu katika jeshi la Burundi ameuwawa usiku wa jana katika hali ya kutatanisha katikati mwa jiji la Bujumbura.

Meja Didier Mihimpundu ameuawa saa chache baada ya kuuawa kwa kamanda wa kambi moja muhimu mjini Bujumbura Kanali Darius Ikurakure akiwa kwenye makao makuu ya jeshi mjini Bujumbura .

Meja Didier Muhimpundu aliuawa karibu saa mbili ya usiku .

Polisi wanasema alipokea simu na kuondoka ndani ya baa moja mjini Bujumbura kabla ya kufyatuliwaa risasi.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Uhasama nchini Burundi ulianza baada ya rais Nkurunziza kutangaza nia ya kuwania muhula wa tatu

Hadi sasa waliomuuwa afisa huyo aliyekuwa msimamizi wa idara ya afya ya jeshi , hawajafahamika kwa mujibu wa naibu msemaji wa polisi Moise Nkurunziza.

'' Meja Muhimupundu alipigiwa simu na mtu akiwa katika baa, halafu alipotoka kutaka kukutana na mtu huyo, wakampiga risasi, na akafariki papo hapo,''

''Uchunguzi umeanzishwa kujua vema watu hao waliofanya ukatili huo , na hivo wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria kuadhibiwa. alisema Nkurunziza.

Saa moja kabla ya Meja Muhimpundu kuuwawa, kulisikika milio ya risasi Kaskazini mwa jiji katika mtaa wa Carama .

Wakaazi sehemu hiyo wanathibitisha polisi mmoja aliuwawa katika ufyatulianaji huo wa risasi.

Image caption Katika kipindi cha miezi minane , maafisa wakuu jeshini wasiopungua watano wameuawa katika jiji la Bujumbura

Hata hivo polisi imekanusha taarifa hizo na kutaja kuwa alitekwa.

'' Polisi huyo alitekwa na watu waliokuwa katika gari la watu binafsi, ambao walikuwa wamevalia sare za kijesh.''

''Taarifa za kuuliwa kwake si sahihi hazina ukweli maana haijaonekana maiti yake'' alisema msemaji wa polisi Nkurunziza.

Awali jana mchana aliuwawa Kamanda wa kambi moja muhimu ya kijeshi hapa nchini Luteni Kanali Darius Ikurakure akiwa ndani ya makao makuu ya jeshi hapa mjini Bujumbura.

Mauaji hayo ya mfululizo yameanza kutafsiriwa kama ulipizanaji kisasi katika jeshi lenye mchanganyiko wa makabila na kutishia uwiano wa vikosi vya ulinzi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mauaji hayo ya mfululizo yameanza kutafsiriwa kama ulipizanaji kisasi katika jeshi

Msemaji wa Jeshi Clement Cimana .ameonya kuhusu hali hiyo'' Makao Makuu ya jeshi yanalaani vikati ukatili wowote wa aina hii,uongozi wa jeshi unawatolea wito wanajeshi popote walipo kubaki wanashikamana na kuwaepuka watu wanaojaribu kuwagawanya kwa lengo la kusambaratisha jeshi la Burundi.''

Katika kipindi cha miezi minane , maafisa wakuu jeshini wasiopungua watano wameuawa katika jiji la Bujumbura, lakini mauaji ya sasa yameibuka baada ya siku kadhaa za utulivu nchini.