Obama amtaka Castro asiiogope Marekani

Cuba Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Obama alikaa Cuba siku tatu

Rais wa Marekani Barack Obama ameeleza matumaini yake kwamba hali ya Cuba itaimarika, kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.

Kiongozi huyo wa Marekani, ambaye ndiye wa kwanza kuzuru Cuba akiwa bado madarakani katika kipindi cha miaka 88, alitoa hotuba hiyo kutoka ukumbi wa Grand Theatre mjini Havana.

Bw Obama alisema alifika Cuba “kuzika masalio ya Vita Baridi” na miongo mingi ya uhasama.

Alimwambia Rais wa Cuba Raul Castro kwamba hafai kuiogopa Marekani na pia hafai kuogopa “usemi wa watu wa Cuba”.

Bw Obama alisema wakati umefika kwa Marekani na Cuba kuacha nyuma yaliyopita na kusonga mbele “kama marafiki na majirani na kama familia, pamoja” kwa siku za usoni zenye ufanisi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jumatatu, viongozi hao walijibizana kwenye kikao na wanahabari

Amewataka raia wa Cuba kuacha nyuma vita vya kifalsafa na kujieleza sio kwa kupinga Marekani bali kwa kujieleza wao binafsi ama raia wa Cuba.

"Licha ya siasa hizi zote, watu ni wale wale na Wacuba ni Wacuba,” alisema.

Aidha, amehimiza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara vilivyowekewa nchi hiyo na Marekani miaka 54 iliyopita. Tamko hilo lilishangiliwa sana na raia wa Cuba.

Ni Bunge la Congress pekee linaloweza kuidhinisha kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

Bw Obama alikamilisha ziara yake ya siku tatu kwa kuungana na Rais Castro kutazama mechi ya besiboli uwanja wa Latinoamericano mjini Havana.

Haki miliki ya picha Getty

Tampa Bay Rays waliilaza timu ya taifa ya Cuba 4-1.

Baada ya kuondoka Cuba, Bw Obama ameelekea Argentina siku ambayo inalingana na maadhimisho ya miaka 40 tangu kutokea kwa mapinduzi yaliyoingiza mamlakani utawala dhalimu wa kijeshi.

Baadhi ya makundi yanapanga maandamano kushutumu Marekani ambayo inadaiwa kusaidia jeshi wakati wa mapinduzi hayo ya 1976.