Urusi: Ulaya iache mzaha ugaidi ni tishio

Image caption Urusi: Ulaya iache mzaha ugaidi ni tishio

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema kwamba mataifa yote ya bara Ulaya yanafaa kuweka kando kile anachokiita mchezo wa kisiasa wa kijiografia na kuanzisha ushirikiano.

Bwana Lavrov anasema laiti ushirikiano ungelikuweko mataifa hayo ya Ulaya yangeweza kukabiliana na ugaidi kama mashambulio ya hivi punde ya mabomu yaliyotikisa mji wa Brussels Ubelgiji.

Bwana Lavrov ameomba kuwepo kwa ushirikiano na umoja dhidi ya vitisho vya kigaidi-- huku akisema kwamba magaidi hawafai kuachiwa nafasi ya kujigamba na kufanya watakalo katika bara Ulaya.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Lavrov anasema laiti ushirikiano ungelikuweko mataifa hayo ya Ulaya yangeweza kukabiliana na ugaidi

Lavrov amesema hayo kabla ya kuanza mazungumzo na mwenzake wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.

Naye Waziri mkuu wa Ufaransa Manuel Valls ameyashutumu mataifa ya bara Ulaya kwa "kufumbia macho" vitisho vya makundi yenye itikadi kali ya kiislamu.

Bwana Valls, ameiambia radio moja ya Ufaransa kuwa, pana haja ya kuongeza ulinzi mkali katika mipaka ya mataifa ya Jumuia ya bara Ulaya ili kuzuia mashambulizi kama ya jana yaliyotokea Brussels-Ubelgiji.