Trump na Clinton washinda mchujo Arizona

Arizona Haki miliki ya picha AFP
Image caption Trump amechukua wajumbe wote Arizona

Wagombea urais wanaoongoza nchini Marekani Donald Trump wa Republican na Hillary Clinton wa Demcratic wamepata ushindi mkubwa katika mchujo jimbo la Arizona.

Suala la uhamiaji ndilo lililotawala sana katika jimbo hilo la kusini magharibi, ambalo ndilo kubwa zaidi miongoni mwa majimbo yaliyofanya mchujo Jumanne.

Kura zilionyesha ujumbe wa Bw Trump wa kupinga wahamiaji ulivutia wapiga kura wahafidhina katika jimbo hilo.

Bi Clinton naye alionekana kuendelea kuvutia makundi ya wachache, akipata kura nyingi kutoka kwa maeneo ya watu wa Hispania.

Wakati wa hotuba ya ushindi Seattle, Bi Clinton alizungumzia shambulio la Brussels na kusema: “Tunahitaji amiri jeshi ambaye anaweza kutoa uongozi, mtu mwenye hekima na thabiti katika kubali tishio hizi.”

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Clinton ameendelea kumshutumu Trump

“Jambo ambalo hatuwezi tukataka ni viongozi wanaochochea wasiwasi zaidi,” alisema akimrejelea Bw Trump.

Mpinzani wa Bi Clinton katika chama cha Democratic Bernie Sanders alitarajiwa kushinda majimbo madogo ya Idaho na Utah.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Trump, Clinton, Cruz na Sanders.

Seneta wa Texas Ted Cruz naye anatarajiwa kushinda mchujo wa Republican Utah.

Katika jimbo la Arizona, mshindi alikuwa anachukua wajumbe wote maana kwamba Bw Trump amejiongezea wajumbe 58.