CCM yapata wabunge wawili wapya Tanzania

Lubuva
Image caption Jaji Mstaafu Damian Lubuva

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania imewatangaza wabunge watatu watakaoshikilia viti vitatu maalum vya wanawake katika bunge la Tanzania ambavyo vilikuwa vimebaki wazi.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewapata wabunge wawili, Ritha Enespher Kabati na Oliver Daniel Semuguruka, nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikapata mbunge mmoja, Lucy Fidelis Owenya.

Viti hivyo viliachwa wazi wakati wa uteuzi wa wabunge maalum Novemba mwaka jana kusubiri majimbo manane ambayo uchaguzi wake ulikuwa umeahirishwa kwa sababu mbalimbali.

Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema vyama hivyo viwili ndivyo pekee vilivyotimiza viwango vya kushirikishwa kwenye uteuzi wa wabunge hao maalum.

Kati ya jumla ya wabunge 113 maalum wanawake, CCM sasa itakuwa na wabunge 66, Chadema wabunge 37 na Chama cha Wananchi (CUF) wabunge 10.

Wabunge hao waliteuliwa kwa kufuata mtiririko wa orodha iliyowasilishwa kwa tume na katibu wa chama husika.