Mlipuko wazua taharuki chuo kikuu Kenya

Bweni Haki miliki ya picha Moi University Facebook
Image caption Bweni la wanafunzi katika bewa kuu la Chuo Kikuu cha Moi

Wanafunzi 22 kutoka Chuo Kikuu cha Moi, magharibi mwa Kenya wanauguza majeraha baada ya kuumia kufuatia taharuki iliyotokana na mlipuko chuoni.

Mlipuko mkubwa ulitokea katika bweni la wanafunzi nambari D Jumatano jioni na baadhi ya wanafunzi waliodhani lilikuwa shambulio la kigaidi walikimbia, baadhi wakiruka kutoka vyumba vyao kupitia madirisha.

Chuo hicho kinasema mlipuko huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.

Wanafunzi katika bweni jirani nambari G ambao hawakufahamu kuhusu hitilafu hiyo walijawa na wasiwasi hasa baada ya mwanafunzi mmoja kusema “Al-Shabaab” kwa sauti.

Haki miliki ya picha Moi University Facebook
Image caption Afisa aonesha mtambo uliolipuka katika bweni

“Wanafunzi waliojawa na wasiwasi waliruka kupitia madirisha kujiokoa. Wanafunzi watatu kutoka bweni D na 19 kutoka Bweni G waliumia,” chuo hicho kilisema kupitia ujumbe kwenye Facebook.

"Wanafunzi 11 kati ya hao wamepelekwa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret kwa matibabu zaidi. Hao wengine walitibiwa katika zahanati chuoni na kuruhusiwa kuondoka.”

Haki miliki ya picha Moi University Facebook
Image caption Mtambo wa umeme uliolipuka

Mlipuko huo ulitokea mwendo wa saa kumi na mbili kasoro dakika ishirini jioni.

Aprili mwaka jana, wanafunzi 147 waliuawa katika Chuo Kikuu cha Garissa, mashariki mwa Kenya baada ya wanamgambo wa al-Shabab kushambulia chuo hicho.

Chuo hicho kilifunguliwa tena Januari mwaka huu.