Al jazeera kuwafuta kazi 500

Image caption Al Jazeera imefunga kituo chake nchini Marekani

Shirika la utangazaji la kimataifa, la Al-Jazeera, litawafuta kazi wafanyikazi wake kama 500, nyingi kati ya nafasi hizo zitakazofungwa zipo katika makao yao makuu huko Doha Qatar.

Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo inasema, kazi zinapunguzwa ili "kutumia vema wafanyakazi walioko".

Wadadisi wanasema, sababu ni kuanguka kwa bei ya mafuta kimataifa, kwani serikali ya Qatar ndiyo inayogharimia Al-Jazeera.

Tangazo limetolewa miezi miwili baada ya Al-Jazeera kusema kuwa itafunga matangazo yake Marekani.

Kaimu mkurugenzi mkuu Mostefa Souag alisema japo wanahuzunika kuwapoteza wafanyikazi wema hatua hiyo ni sharti ichukuliwe kwa nia ya kuendeleza mapato ya shirika hilo.

Al Jazeera, inayogharamiwa na serikali ya Qatar ilianzishwa mwaka wa 1996 na inavituo katika mataifa 70 kote duniani.