Aliyesaidia El Chapo kulangua pesa anaswa

Guzman Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Guzman alikamatwa Januari nchini Mexico

Maafisa wa usalama nchini Mexico wamemkamata mwanamume wanayesema alisaidia kulangua pesa kwa niaba ya mlanguzi wa mihadarati Joaquin Guzman, aliyejulikana sana kama "El Chapo" au "Shorty".

Juan Manuel Alvarez Inzunza, kwa jina la utani "King Midas", alikamatwa akiwa likizoni katika jimbo la Oaxaca, kusini mwa nchi hiyo.

Guzman, kiongozi wa zamani wa genge la Sinaloa, kwa sasa anasubiri kuhamishiwa Marekani akajibu mashtaka.

Alikamatwa Januari baada yake kutoroka jela mwaka jana.

Haki miliki ya picha Other

Bw Inzunza anashukiwa kulangua takriban $300m-$400m kwa niaba ya genge la Sinaloa kupitia mtandao wa kampuni na vituo vya kubadilisha pesa za kigeni.

Mahakama ya dola mjini Washington iliomba Inzunza akamatwe na huenda akapelekwa Marekani kujibu mashtaka.

Guzman mwenyewe anatakiwa Marekani akajibu mashtaka ya ulanguzi wa mihadarati California, na mauaji Texas.