Sharif aahidi kuangamiza magaidi Pakistan

Shambulio Haki miliki ya picha AP
Image caption Watu 70 walifariki kwenye shambulio hilo

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif ametoa wito kwa kuwepo ushirikiano zaidi kati ya idara za usalama nchini humo ili kukabiliana na ugaidi.

Amesema hayo siku moja baada ya watu zaidi ya 70 kuuawa kwenye shambulio la bomu katika mji wa Lahore. Kiongozi huyo ameahidi kuwaangamiza magaidi hao.

Bw Sharif, aliyekutana na viongozi wa idara za usalama, amesema taifa hilo litaimarisha juhudi za kukabiliana na ugaidi.

Watu kadha wamekamatwa na silaha kupatikana kwenye operesheni iliyofanywa na vikosi vya usalama, jeshi limesema.

Kundi la Jamaat-ul-Ahrar lililotokana na kundi la Taliban limekiri kutekeleza shambulio hilo.

Watu 300 walijeruhiwa na maafisa wa serikali wamesema idadi ya waliofariki inatarajiwa kupanda.

Eneo hilo lilikuwa na watu wengi kuliko kawaida, kwani Wakristo walikuwa wamekusanyika katika bustani kusherehekea Pasaka.

Hata hivyo, wengi wa waliofariki walikuwa Waislamu.

Mmoja wa waliofariki, mvulana Mkristo Sahil Pervez, alizikwa Jumatatu.

Bw Sharif alitembelea majeruhi hospitalini.

Image caption Mazishi ya mmoja wa waliofariki Lahore

Baadaye katika mkutano na maafisa wa usalama, alisema ni jambo la umuhimu mkubwa kuwashinda magaidi.

“Azma yetu kama taifa na serikali inaendelea kuwa thabiti na adui huyu mwenye uoga anajaribu kushambulia watu wasio na silaha,” amesema.

Aliapa kuwa serikali yake itawaangamiza magaidi hao walioua “wanangu”.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis kwa upande wake ametoa wito kwa serikali ya Pakistan kulinda makundi ya kidini ya wachache nchini humo.