Mwanamume aliyeteka ndege ya Misri akamatwa

Ugaidi Haki miliki ya picha Getty
Image caption Maafisa wanasema kisa hicho hakikuwa na uhusiano na ugaidi

Mwanamume aliyeteka nyara ndege ya shirika la Misri la EgyptAir na kuishurutisha kutua Cyprus amekamatwa, wizara ya mashauri ya kigeni ya Cyprus imetangaza.

Mwanamume huyo alidai kwamba alikuwa na mkanda wa kujilipua na kumwamuru rubani wa ndege hiyo kuielekeza Cyprus au Uturuki.

Ndege hiyo, iliyokuwa safarini kutoka Alexandria hadi mjini Cairo, mwishowe ilitua uwanja wa Larnaca nchini Cyprus.

Abiria karibu wote walikuwa wamefanikiwa kuondoka kutoka kwenye ndege hiyo.

Ripoti zinasema kuwa mtekaji wa ndege ya EgyptAir anataka kuongea na mkewe walietengana naye anayeishi Cyprus ambaye kwa sasa anadaiwa kuelekea katika uwanja huo wa ndege.

Rais wa Cyprus Nicos Anastasiades amewaambia waandishi wa habari kwamba tukio hilo la utekaji nyara halikuwa la kigaidi.

Akijibu maswali ya waandishi iwapo mtekaji huyo alishinikizwa na mapenzi, alicheka na kusema, ''kila mara kuna mwanamke anayehusishwa''.

Shirika la habari la Cyprus CYBC linasema kuwa mtekaji huyo huenda alikuwa na malengo yake ya kibinafsi, mtekaji huyo alikuwa na mkewe waliyetengana nchini Cyprus.

Walioshuhudia wanasema kuwa mtekaji huyo alirusha barua katika uwanja huo wa ndege ilioandikwa Kiarabu akiomba ipelekwe kwa mwanamke huyo.