Ndege ya Misri iliyotekwa yatua Cyprus

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ndege ya kampuni ya EgyptAir

Ndege moja ya shirika la ndege la EgyptAir imetekwa nyara na kulazimishwa kutua katika uwanja wa ndege wa Larnaca kusini mwa pwani ya taifa la Cyprus.

Ndege hiyo MS181,airbus A320 iliokuwa ikiwabeba abiria 81 kutoka Alexandria kuelekea Cairo ilitekwa nyara baada ya abiria mmoja kusema amevaa ukanda wa mlipuaji wa kujitolea mhanga .

Shirika hilo la ndege limesema kuwa majadiliano yamesababisha kuwachiliwa huru kwa abiria wote waliokuwa ndani isipokuwa wafanyakazi wa ndege hiyo na abiria wanne wa kigeni.

Kanda ya video iliochukuliwa imeonyesha watu wakiondoka katika ndege hiyo na kupanda basi.

Uwanja wa ndege wa Larnaca umefungwa huku ndege zilizokuwa zikisubiriwa kutua zikielekezwa kwengineko.

Rubani anasema kuwa abiria mmoja alimwambia alikuwa amevaa nguo ya ndani iliojaa vilipuzi na kuilazimisha ndege hiyo kutua katika uwanja wa ndege wa Larnace,kulingana na taarifa ya wizara ya uchunkuzi wa angani nchini humo.

''Habari tulionayo kufikia sasa ni kwamba mtekaji huyo ni mmoja ,mtu huyo hajataka chochote '',afisa wa wizara ya maswala ya kigeni nchini humo Alexandros Zenon aliiambia runinga ya Ufaransa.