Magufuli aahidi kupunguza kodi kwa Watanzania

Magufuli Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Magufuli amesema Tanzania inafaa kujitegemea

Rais wa Tanzania John Magufuli ameahidi kwamba kuanzia bajeti ijayo kodi katika mishahara kwa wafanyakazi itapungua kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9.

Aidha, amesema ataweka kiwango cha kima cha juu na kwamba wale wote wanaopokea mishahara ya hadi shilingi milioni 40, itapunguwa na haitazidi milioni 15

Rais Magufuli ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara Kaskazini Magharibi mwa Tanzania (Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita) ambapo amewataka wananchi wafanya kazi kwa bidii ili kuondokana na tabia ya utegemezi wa misaada ya nje.

"Ni lazima tujisimamie sisi wenyewe. Na tukijisimamia sisi wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi kwelikweli. Kama ni mkulima afanye ukulima kweli kweli, kama ni mfanyabiashara afanye biashara kweli kweli, kama ni mfugaji afuge kweli kweli, kama ki mvuvi avue kweli kweli, Tanzania hii tutavuka," amesema Magufuli.

Awali, Dkt Magufuli, aliagiza kufunguliwa kwa barabara ya Uwanja wa Ndege Mwanza-Igombe hadi Kayenze yenye urefu wa kilomita 7.

Barabara hiyo ilifungwa kupisha upanuzi wa uwanja huo tangu mwaka 2014.

"Nafahamu suala linalowaumiza wananchi la kufungwa kwa barabara ya Airport-Igombe yenye urefu wa kilomita 7, sasa naagiza kuanzia sasa kufunguliwa kwa barabara hiyo ili wananchi watumie kupita ili kuondoa usumbufu wa kuzunguka kule maeneo ya Nyakato hadi maeneo ya TX Kata ya Bugogwa, Kata ya Sangabuye,”alisema.