Rais mpya wa Myanmar aapishwa

Kyaw
Image caption Htin Kyaw ndiye rais wa kwanza wa kiraia Myanmar katika miaka 50

Rais mpya wa Myanmar, Htin Kyaw, ameapishwa na kuwa kiongozi wa kwanza wa kiraia wa nchi hiyo katika kipindi cha miaka 50.

Sherehe ya kumuapishwa imeandaliwa katika mji mkuu wa Naypyidaw, ikiwa ndiyo hatua ya kukamilisha shughuli ya mpito tangu chama cha National League for Democracy kishinde uchaguzi mkuu mwezi Novemba.

Htin Kyaw, ambaye ni rafiki wa karibu wa kiongozi mtetezi wa demokrasia wa chama cha Aung Suu Kyi, amechukua hatamu kutoka jenerali wa zamani Thein Sein, ambaye amesifiwa sana kwa kufanikisha shughuli ya mpito kutoka kwa uongozi wa kijeshi hadi uongozi wa kiraia.

Image caption Bi Suu Kyi ameteuliwa kuwa waziri

Aung San Suu Kyi haruhusiwi kuwa rais kwa mujibu wa katiba ya Myanmar, ambayo zamani ilijulikana kama Burma, lakini amesema wazi kwamba atakuwa na mamlaka makuu.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, alisema alikusudia kuwa “juu ya rais”.

Rais huyo mpya amemteua Suu Kyi kuwa waziri anayesimamia wizara nne.