Assad apendekeza serikali mseto Syria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Bashar al Assad apendekeza serikali mseto Syria

Rais wa Syria amesema kuwa 'maafisa kadhaa wa upinzani' huenda wakajiunga na serikali mseto iwapo mapendekezo yake yatakubaliwa na wajumbe wanaoshiriki katika mazungumzo ya amani huko Geneva Uswisi.

Rais Bashar al-Assad amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Urusi akisema kuwa anatarajia Wanajeshi watiifu kwa serikali yake kujiunga na waasi na wajumbe wa upinzani .

Hata hivyo anasisitiza muundo wa serikali hiyo sharti ukubaliwe huko Geneva ambapo mazungumzo ya amani yanapangwa.

Mazungumzo hayo ambayo sio ya moja kwa moja yalirejelewa mwezi huu.

Hata hivyo haijulikani iwapo kauli ya bw Assad itakubaliwa na upinzani ambao umekuwa ukisisitiza kuwa unamtaka ajiuzulu mamlaka.

Haki miliki ya picha
Image caption Upinzani umekuwa ukisisitiza kuwa unamtaka ajiuzulu mamlaka.

Bw Assad na washirika wanaomuunga mkono, wamesisitiza kuwa kauli ya kumng'oa mamlakani sio hata mada ya kujadiliwa kabisa katika mazungumzo hayo, yeye anasisitiza kuwa hatima yake iko mikononi mwa raia wa Syria.

Msemaji wa upinzani katika meza ya mazungumzo huko Geneva tayari amepuzilia mbali usemi huo wa rais Assad.

Serikali itakayoundwa na ile inayojadiliwa hapa katika mazungumzo haya haina uhusiano wa aina yeyote na rais Bashar al Assad,'' alisema George Sabra ambaye ndiye msemaji wa wapatanisishi.

''Kwa hakika alichosema rais Assad hakina msingi wowote katika mazungumzo haya ya kisiasa'' aliongezea kusema.

Washirika wa pande zote hasimu wanakiri kuwa ilikutafuta amani ya kudumu nchini Syria lazima kuwepo na serikali ya mpwito na hatimaye uchaguzi mkuu na ule wa urais nchini humo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Serikali ya Syria imekataa kabisa kuwatambua waasi kama wapinzani

Hata hivyo kufikia sasa mazungumzo yanayoendeshwa na umoja wa mataifa huko Geneva hayaonekani kuwa na matumaini ya kuleta matunda hivi karibuni.

Lakini bw Assad akizungumza na shirika la habari la Urusi RIA Novosti, anasisitiza kuwa muundo wa serikali ya mseto unatarajiwa kuafikiwa katika mazungumzo hayo ya Geneva.

Serikali ya Syria imekataa kabisa kuwatambua waasi kama wapinzani ikishikilia kuwa kwa sababu wanabeba silaha basi wao ni magaidi.

Rais Assad anasema kuwa katiba kielelezo itawasilishwa katika kipindi cha majuma machache yajayo kisha ipigiwe kura na wasyria.