Trump amtetea meneja wake aliyeshtakiwa

Lewandowski Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bw Lewandowski akiwa na Bw Trump

Mgombea urais anayeongoza katika chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amemtetea meneja wake wa kampeni ambaye ameshtakiwa kumdhulumu mwanahabari wa kike.

Bw Corey Lewandowski tayari ameshtakiwa, na duru zinasema anapanga kukanusha mashtaka hayo. Akiongea na wanahabari, Bw Trump ametoa wito kwa Bw Lewandowski kutokubali kutatua kesi hiyo na Michelle Fields nje ya mahakama.

Kanda ya video iliyotolewa na maafisa wa polisi inamuonesha Bw Lewandowski akimvuta mwanahabari huyo na kumuondoa karibu na Bw Trump mwanahabari huyo alipojaribu kumuendea mgombea huyo wa urais katika kikao na wanahabari jimbo la Florida akitaka kumuuliza swali.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bw Lewandowski anapanga kukanusha mashtaka

Polisi wamemfungulia Bw Lewandowski mashtaka ya kumshambulia mwanahabari huyo, wakisema alimuumiza mkono.

Bw Trump amesema huo ni ukiukaji wa haki akisema polisi hawakumhoji Bw Lewandowski wakati huo.

Mgombea urais anayeshindana na Bw Trump, Ted Cruz, amesema kisa hicho ni ishara tu ya utamaduni wa dhuluma ambao umo kwenye kampeni ya Bw Trump.