Aliyemfanyia utani Nkurunziza akamatwa

Image caption Utani ulimuonyesha Nkurunziza akikataa kuondoka uwanjani licha ya kuonyesha kadi mbili za manjano.

Mchekeshaji mmoja maarufu nchini Burundi amekamatwa kwa kumfanyia utani Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza.

Mchekeshaji huyo anayefahamika kama Kigingi alifanya utani mwaka uliopita, ulioonyesha bwana Nkurunziza akikataa kuondoka uwanjani licha ya kuonyesha kadi mbili za manjano.

Utani huo ulihashiria Rais kuwania muhula wa tatu hatua iliyosababisha miezi kadha ya ghasia.

Kigindi alikamatwa akiwa hotelini mapema wiki hii. Familia yake inasema inahofu kuwa huenda akateswa. Afisa mmoja wa serikali hata hivyo amesema kuwa ataachiliwa hivi karibui.