Kenya Airways kuwafuta kazi wafanyikazi 600

Image caption Kenya Airways

Wafanyikazi 600 wa Shirika la Ndege la Kenya, Kenya Airways watapoteza kazi zao katika juhudi za kulichepua shirika hilo. Kenya Airways ilitangaza hasara ya dola milioni 270 mwaka uliopita, ikiwa ndio hasara kubwa zaidi kuripotiwa na kampuni nchini Kenya.

Likijulikana kama Fahari ya Afrika, hakuna cha kufurahia tena katika shirika la Ndege la Kenya.

Makali ya hasara yalioripotiwa na kampuni hiyo sasa yameanza kuwalenga wafanyikazi wake ambapo mamia wanatarajiwa kupigwa kalamu.

Kenya Airways pia imesema hatua hiyo ni katika juhudi za kurejesha mabawa yake tena katika safari za ndege barani Afrika.

Watakaoponea kutemwa nje huenda wakajipata katika kazi nyingine ambazo hawakuzoea.

Mamlaka za shirika hilo zinakabiliwa na changamoto ya kurejesha imani kwa wawekezaji na wenye hisa ambao wamelalamikia kwamba huenda shirika la Ndege la Kenya linatumbukia kwenye kaburi la sahau.

Mpango mpya wa kufufua Kenya Airways maarufu kama 'operation pride' unaolenga kuokoa kima cha dola milioni 200, pamoja na kupunguza gharama za kufanyia kazi.

Aidha kampuni niyo itauza baadhi ya ndege zake ambapo imeafikiana mkataba na kampuni ya ndege kutoka Marekani Omni Air International kuuza ndege mbili aina ya Boeing.