Ndege za Marekani zashambulia al-Shabab

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ndege ya kivita Marekani

Jeshi la Marekani limesema kuwa limetekeleza shambulizi kwa kutumia ndege isiokuwa na rubani nchini Somalia, ikilenga gari moja lilokuwa limewabeba wanachama watatu wa kundi la kigaidi la al-Shabab.

Kulingana na msemaji wa pentagon, aliyelengwa hasa ni Hassan Ali Dhoore ambaye anatuhumiwa kuandaa mashambulizi ya hivi karibuni ya mabomu katika uwanja wa ndege wa Mogadishu na katika hoteli moja ambapo raia wa Marekani waliuwawa.

Shambulio hilo la majeshi ya Marekani limetekelezwa katika eneo la kaskazini mwa mji wa Jilib, karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, huku Marekani ikisema ingali inatathmini matokeo ya shambulio hilo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa al-Shabab

Shambulizi hilo la hivi karibuni la Marekani linajiri wiki chache baada ya shambulizi jingine katika kambi ya mazoezi ya al-Shabab kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani na nyingine iliokuwa na rubani.