Milio ya risasi yasikika Congo-Brazzaville

Denis Sassou Nguesso Haki miliki ya picha AFP
Image caption Denis Sassou Nguesso ni miongoni mwa marais walioongoza muda mrefu zaidi Afrika

Milio ya risasi imesikika katika barabara za mji mkuu wa Jamhuri ya Congo, Brazzavile na wanajeshi wametumwa katika barabara za mji huo.

Watu walioshuhudia wameambia BBC kwamba kambi ya jeshi ilishambuliwa mapema Jumatatu.

Afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe ameambia shirika la habari la AP kwamba polisi wanakabiliana na kundi linaloitwa Ninja.

Hayo yamejiri wiki kadha baada ya Denis Sassou Nguesso kushinda muhula wa tatu kwenye uchaguzi ambao ulikosolewa na viongozi wa upinzani.

Bw Sassou Nguesso amekuwa madarakani tangu 1979, kipindi pekee ambacho hakuwa madarakani kikiwa ni miaka mitano baada ya kushindwa uchaguzi wa 1992.

Upinzani umesema kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika uchaguzi uliofanyika mwezi Machi.

Shirika la habari la Reuters limesema vijana wafuasi wa upinzani wameandamana wakiimba "Sassou, ondoka!"

Wanadaiwa kuteketeza afisi za meya na makao makuu ya polisi katika eneo la Makelekele.

Taifa la Congo limekabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mapigano ya waasi awali.

Ninjas walikabiliana na wanajeshi wa serikali wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 1997 na 1999.

Walikuwa waaminifu kwa Waziri Mkuu wa zamani Bernard Kolelas na walitia saini mkataba wa amani na serikali 2003.