Waziri Kiongozi mwanamke Kashmir aapa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waziri Kiongozi wa Jimbo la Kashmir Mehbooba Mufti ni mwanamke wa kwanza kuchukua nafasi hiyo

Mehbooba Mufti ameapishwa na kuwa mwanamke wa kwanza kuchukua madaraka ya Waziri kiongozi wa jimbo la Kashmir nchini India

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 56 ni mtoto wa waziri kiongozi wa zamani, Mufti Mohammed Sayeed aliyefariki mwezi Januari.

Kifo cha Baba yake kilisababisha hali ya mvutano kati ya Mehbooba na Chama tawala nchini India,BJP kuhusu mustakabali wa serikali ya pamoja.

Wachambuzi wa mambo wanasema Bi Mufti anaweza kukumbana na changamoto ndani ya Chama chake, na pia kutoka chama kilichoundwa kutokana na muungano wao.

Bi Mufti ameapa baada ya kuchelewa kwa mchakato huo kwa takriban miezi mitatu tangu baba yake aage dunia.

Mkutano na Waziri Mkuu, Narendra Modi tarehe 23 mwezi Machi hatimaye uliuhuisha tena umoja huo ambao ulikuwa na vyama viwili vinavyokinzana, Chama cha Bi Mufti, Peoples Democratic Party (PDP) na Bharatiya Janata Party (BJP).

Mwaka jana, Bwana Sayeed aliuita muungano wa vyama hivyo kuwa ni muungano wa pembe ya kaskazini na kusini.