Uchunguzi: Viongozi 18 wa Afrika waliotajwa

Image caption Naibu jaji mkuu wa Kenya bi Kalpana Rawal

Viongozi na watu wengine maarufu 18 wa Afrika wametajwa katika nyaraka zilizofichuliwa hapo jana zikiwahusisha na kampuni moja ya kisheria nchini Panama inayowasaidia kufungua kampuni katika mataifa yasiotoza kodi kwa minajili ya kukwepa kodi, utakatishaji fedha, kukiuka mikataba na vikwazo vya kiuchumi kimataifa.

Kwa mujibu wa nyaraka za siri zilizopatikana na gazeti moja la Kijerumani na kusomwa na Idhaa ya BBC, kampuni hiyo ya Mossack Fonseca imewasaidia viongozi hao wa Afrika washirika wao na jamaa zao wamekuwa wakiitumia kampuni hiyo kuficha asili ya mali yao.

Hati hizo zinaonyesha kuwa mabilioni ya pesa zilitolewa barani Afrika na kuwekezwa katika kampuni hewa ughaibuni.

Kwa baadhi yao akiwemo rais wa zamani wa Sudan Ahmad Ali al-Mirghani, na Naibu jaji mkuu wa Kenya bi Kalpana Rawal, na mwanaye aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, Kojo Annan kampuni hizo hewa zilitumika kununua nyumba katika mitaa ya kifaharai mjini London Uingereza.

Msaidizi wa karibu wa Mfalme wa Morocco Mounir Majidi -alitumia kampuni kama hiyo kununua mashua ya kifahari mwaka wa 2006.

Mawakili wake wanasema kuwa biashara hiyo ilikuwa halali.

Mpwa wa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ,Khulubuse Zuma ametajwa kama mmiliki wa kampuni iliyotwaa hati ya kuchimba mafuta katika maeneo mengi ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo mwaka wa 2010.

Haki miliki ya picha PA
Image caption James Ibori aliyekuwa gavana wa jimbo la Delta anatumikia kifungo gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kutakatisha fedha 2012

Msemaji wake amekanusha kuwahi kumiliki kampun hewa.

Viongozi wengine na jamaa zao walikataa mwito wa BBC wa kuwataka wajieleze.

James Ibori aliyekuwa gavana wa jimbo la Delta anatumikia kifungo gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kutakatisha fedha mnamo mwaka wa 2012.

Kampuni hewa 4 zinazohusiana naye zilitumika kutakatisha fedha ambazo baadhi zilitumika kununua ndege ya kibinafsi iliyogharimu takriban dola milioni $20,000,000.