Suu Kyi aachilia wizara mbili Myanmar

Wizara Haki miliki ya picha AP
Image caption Suu Kyi ataendelea kuwa waziri wa mambo ya nje na waziri katika afisi ya rais

Kiongozi mtetezi wa demokrasia nchini Myanmar Aung San Suu Kyi amekubali kuachilia wizara mbili kati ya nne alizokuwa amepewa serikalini.

Amechukua hatua hiyo chini ya wiki moja baada ya serikali ya kiraia kuapishwa.

Suu Kyi ameachilia wizara za kawi na elimu, lakini ataendelea kuwa waziri wa mashauri ya mambo ya nje na waziri katika afisi ya rais.

Kumekuwa na mipango ya kumpa wadhifa mpya wa mshauri mkuu wa serikali, wadhifa ulio na majukumu sawa nay a Waziri Mkuu.

Mwandishi wa BBC nchini Myanmar, ambayo zamani ilifahamika kama Burma, anasema Bunge la Chini nchini humo huenda likapitisha mswada wa kuunda wadhifa huo mpya Jumatatu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Suu Kyi na Rais Htin Kyaw

Baadaye mswada huo utahitaji kutiwa saini na Rais Kyaw kabla ya kuanza kutekelezwa.