Mama ajuta kukataa chanjo ya kifaduro Australia

Cormit Avital Haki miliki ya picha Gold Coast Health
Image caption Cormit Avital anasema hakupokea chanjo ya kifaduro maana alihisi ni mwenye afya

Mama mmoja raia wa Australia amesema anajuta kwa kukataa kupata chanjo ya maradhi ya kifaduro wakati alipokuwa mjamzito baada ya kumuambukiza mwanae maambukizi hayo yanayoweza kumuua.

Cormit Avital amesema kuwa alikataa kupewa chanjo hiyo kwasababu alikua mwenye ''afya, thabiti na ni mtu asiekula nyama".

Alipata maradhi hayo muda mfupi kabla ya kujifungua na kumuambukiza mwanae Eva, ambae ilibidi akae katika chumba cha uangalizi wa dharura cha hospitali kwa mwezi mzima.

Bi Avital alirekodi video akiwaonya watu wengine juu ya masaibu ''yaliyomkumba'' .

" Ingeliwezekana nirejeshe nyuma muda ninejikinga ," alisema, katika video iliyotolewa na taasisi ya Gold Coast Health, mamlaka ya kikanda ya masuala ya afya.

Katika kipindi cha wiki mbili , kikohozi cha mtoto Eva "kimekua cha kupindukia kiasi kwamba anakohoa hadi anabadilika rangi ya mwili na kuwa rangi ya blu, nashindwa hata kumshika mikononi mwangu, hawezi kubumua vizuri ," alisema Avita

"Kwa wakati fulani unafikiria amefia mikononi . Ni mateso makali kwa mtoto mchanga unaempenda sana'' alisema bi Avita

Maradhi ya kifaduro husababishwa na aina ya bakteria wanaojulikana kwa lugha ya kitaalam kama Bordetella pertussis.

Zaidi huwaathiri watoto ambao huwa katika hatari ya kupata matatizo zaidi na hata kufa.

Dalili za awali za kifaduro ni mafua ya kawaida, baadae mgonjwa kuanza kukohoa na hatimae mgonjwa huweza kupata hata kichomi.

Watoto wachanga hubadilika rangi ya mwili na kuwa blue kutokana na kukosa hewa safi ya kupumua ya oxygeni.