Visa vya ugonjwa wa Malaria vyapungua Kenya

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vita dhidi ya Malaria

Ripoti mpya ya Afya nchini Kenya inaonyesha kupungua kwa idadi ya watu wanaoambukizwa ugonjwa wa Malaria kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.

Utafiti huo uliofanywa na wizara ya Afya unasema hali hiyo inatokana na ongezeko la watu wanaolala ndani ya neti pamoja na kupata matibabu ya mapema.

Malaria iliwaua karibu watu nusu milioni duniani mwaka jana, huku vifo tisa juu ya kumi vikitoka kusini mwa Sahara.

Vilevile ugonjwa huo umetajwa kuwa unaosababisha maafa zaidi barani Afrika. Hata hivyo ripoti ya sasa inatoa matumaini katika kuangamiza ugonjwa huu.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ya kusini mwa Jangwa la Afrika ambapo Malaria imeandelea kuangamiza watu.

Hata hivyo visa vya maradhi hayo vimeshuka kwa asili mia nane ikilinganishwa na hali ilivyokua miaka sita iliyopita.

Mafanikio haya yamechangiwa na utumizi wa neti za kukinga mbu pamoja na matibabu ya mapema.

Ripoti imenadi kwa kina jinsi utumizi wa neti umesambaa maeneo yanayoathirika zaidi na Malaria.

Kati ya makaazi kumi, sita yanahakikisha wenyeji wake wanalala chini ya neti ya kukinga mbu.

Aidha wanawake waja wazito na watoto wamekua wakihakikisha wanapokea matibabu punde zinapojitokeza dalili za ugonjwa huo.

Malaria inaongoza katika magonjwa ambayo watu wanatafuta matibabu yake, sawa na maradhi ambayo yanatibiwa na wagonjwa kurudi nyumbani.

Nchini Kenya maeneo ya pwani na Magharibi mwa nchi yameathirika zaidi ya maambukizi ya Malaria, ambapo watoto watatu kati ya kumi hupatikana na maradhi hayo.