Brazzaville:Kiongozi wa upinzani ahofia usalama wake

Haki miliki ya picha
Image caption Kiongozi wa upinzani, Jean-Marie Mokoko

Kiongozi wa upinzani nchini Congo-Brazzaville ameiambia BBC kuwa makazi yake yaliyo mjini Brazzaville, yamezungukwa na vikosi vya usalama kwa kipindi cha siku nne zilizopita na kuwa anahofia usalama wake.

Jean-Marie Mokoko amesema ulinzi aliokuwa nao kama aliyekuwa Mkuu wa zamani wa majeshi umeondolewa.

Msemaji wa Polisi amekataa kuthibitsha au kukataa madai hayo.

Bwana Mokoko ambaye aliwahi kuwa mtu wa karibu kwa Rais Denis Sassou Nguesso aliwania Urais mwezi uliopita na kuibuka nafasi ya tatu.

Mokoko alikataa matokeo ambayo Sassou Nguesso alishinda kwa asilimia 60 ya kura baada ya kufanyika mabadiliko ya katiba yaliyoruhusu kuwania muhula wa tatu.

Vyama vyote vikuu vya upinzani vimesema uchaguzi ulikua wa udanganyifu, ingawa Guy-Brice Kolelas, aliyekuwa mshindi wa pili alikubali kushindwa, akisema ingawa kulikua na dosari za kila namna hakutaka kuwepo kwa vurugu zozote.

Siku ya jumatatu Mamlaka zilishutumu kundi la wanamgambo wa Ninja, ambalo liliwahi kuwepo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1997-1999 kushambulia majengo ya serikali mjini Brazzaville