Watu 11 wajaribu kujiua siku moja Canada

Trudeau Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Trudeau amesema habari hizo ni za kuvunja moyo

Jamii moja ya watu asilia kaskazini mwa Canada imetangaza hali ya hatari baada ya watu 11 kujaribu kujitoa uhai siku moja.

Watu 28 walijaribu kujiua katika jamii hiyo ya kabila la First Nation, Attawapiskat eneo la Ontario mwezi Machi, vyombo vya habari Canada vinasema.

Tangu Oktoba, watu zaidi ya mia moja wamejaribu kujitoa uhai. Mmoja alifariki.

Waziri mkuu Justin Trudeau, amezitaja habari hizo kuwa za ‘kuvunja moyo.’

Raia wa kiasili nchini Canada ambao ni takriban milioni 1.4 huishi katika ufukara.

Muda wao wa wastani wa kuishi huwa chini kuliko muda wa wastani wa kuishi miongoni mwa raia wa Canada.

Bruce Shisheesh, chifu wa jamii ya Attawapiskat amesema watu 11 walijaribu kujitoa uhai Jumamosi, jambo lililomfanya kutangaza siku ya hatari.

Serikali inayosimamia watu wa kabila la First Nation imetuma maafisa wa dharura Attawapiskat tangu kutangazwa kwa hali ya tahadhari. Watu takriban 2,000 huishi eneo la Attawapiskat.

Shirika la afya la Canada, limesema katika taarifa yake kwamba limetuma washauri wawili wa maswala ya kiakili kutoka kwa kitengo hicho.

Mbunge wa eneo hilo, Charlie Angus amesema: "Hili ni tatizo kubwa linaloathiri jamii hii.”

Haki miliki ya picha AP
Image caption Trudeau akiwa eneo la Quebec

Amesema ngazi zote za serikali hazijachukua hatua zozote za maana.

"Tutaendelea kufanya juhudi ili kuimarisha hali ya raia kwa watu asilia,” Waziri mkuu Trudeau alisema.

Jamii nyingine mkoa Manitoba, magharibi mwa Canada ilitoa wito kwa serikali ya taifa kuisaidia baada ya watu sita kujiua katika kipindi cha miezi miwili.

Watu 140 walijaribu kujiua katika kipindi cha wiki mbili.