Rais Rousseff amshutumu makamu wake

Haki miliki ya picha Ag. Brasil
Image caption Rais wa Brazil, Dilma Rousseff

Rais wa Brazil Dilma Rousseff, amemlaumu makamo wake kwa kupanga kuuangusha utawala wake hivyo kumuita msaliti.

Rais Rousseff, ambae anakabiliwa na kura ya kumuondoa madarakani inayotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili, amesema makamo wa rais Michel Temer anapanga njama na spika wa bunge kumuondoa rais aliyechaguliwa kwa njia halali.

Amesema siri yao imefichuka pale ujumbe wa sauti ulipotolewa siku ya Jumatatu ambapo bwana Temer amesikika akiifanyia mazoezi hotuba ambayo angeitoa pindi rais Rousseff ameondolewa madarakani.

Ofisi ya rais Rousseff imesema makamo wake anatakiwa ajiuzulu iwapo rais atafanikiwa kukwepa kuondolewa madarakani.

Akizungumza kwa hasira katika mji mkuu wa Brasilia, Rais amesema maadui zake hivi sasa wanajaribu wazi wazi kuisambaratisha serikali iliyopo madarakani.