Mfumo wa kisasa wa uchukuzi wazinduliwa Rwanda

Kadi
Image caption Kadi hizo zinatumiwa na kampuni mbili za mabasi

Nchini Rwanda abiria wanaotumia usafiri wa mabasi mjini Kigali wameanza kusafiri kwa kutumia mfumo mpya wa kadi za elektroniki kwa kulipia nauli.

Mfumo huu umewakosesha kazi makondakta huku ukikaribishwa na wamiliki wa kampuni za mabasi ya abiria kwa kuwasaidia kudhibiti wizi wa pesa uliokuwepo.

Mwandishi wa BBC aliyeko Kigali Yves Bucyana anasema kila abiria aliye na kadi anauingia ndani ya basi na kubonyeza kadi yake kwenye mashine maalum iliyobandikwa karibu na mlango wa basi.

Huo ni mfumo mpya,unaotumiwa na makampuni mawili tu miongoni mwa makampuni kadhaa ya mabasi ya abiria mjini Kigali.

Image caption Mashine ya kusoma kadi mlangoni

Kwa mabasi yaliyoanza kutumia kadi,watu wa kwanza kuathirika ni wapiga debe ambao wameachishwa kazi.

Baadhi ya madereva nao hawajaushabikia mfumo huo wa kulipia nauli kwa kutumia kadi za elektroniki.

“Tuliingia hasara kwa kupungukiwa na abiria. Hata baadhi ya abiria walikataa kununua kadi hizi wakisema kamwe hawawezi kutumia kadi hizo kwa madai kuwa ni kadi za illuminati,” alisema dereva mmoja.

Kampuni zinazotumia mfumo huo zinausifu kwa kuwa uliwawezesha kudhibiti wizi wa fedha kwani baadhi ya watumishi walikuwa wakighushi tiketi zilizokuwa zinatumiwa.

Image caption Kadi hizo zinagharimu nusu dola

Bei ya kadi moja ni franka za Rwanda 500 ama nusu ya dola moja ya Kimarekani.

Kisha abiria hulipia kila safari anayoifanya.

Kwa kuwa siyo abiria wote walio na kadi hizi, malipo ya hapo kwa hapo nayo bado yanakubalika.

Mfumo huu umekuja kuimarisha azma ya serikali ya Rwanda kuwahimiza raia kulipia huduma muhimu kwa kutumia njia ya elektroniki.