Obama asema Islamic State wanakimbilia Libya

Obama Haki miliki ya picha EPA
Image caption Obama majuzi alisema utawala wake ulifanya kosa kubwa Libya

Rais wa Marekani Barack Obama amesema wapiganaji wa kundi linalojiita Islamic State (IS) wanelekea Libya kwa wingi baada ya kukabiliwa vikali Iraq na Syria.

Hata hivyo amesema Marekani itaendelea na juhudi za kupambana na kundi hilo hata nchini Libya.

Akiongea baada ya mkutano na wakuu wa usalama katika makao makuu ya CIA, Bw Obama amesema idadi ya wapiganaji wa IS Iraq na Syria imeshuka mno tangu kuanza kwa operesheni ya majeshi ya mataifa 66 inayoongozwa na Marekani.

"Kwa sababu sisi, na washirika wetu, tumeifanya vigumu kwa wapiganaji kutoka nje kufika Syria na Iraq, tumeshuhudia ongezeko la wapiganaji wa IS wanaoelekea Libya,” Bw Obama amesema.

"Tutaendelea na juhudi zetu za kuwakabili kutoka Libya huku tukisisitiza kwamba serikali mpya ya Libya inafanya kazi kuhakikisha nchi hiyo iko salama,” ameongeza.

Image caption Gaddafi aliuawa mwaka 2011

Wiki iliyopita, Bw Obama alisema kosa kubwa alilolifanya wakati wa utawala wake ni kukosa kuwa na mpango mzuri kwa maisha Libya baada ya kuondolewa mamlakani kwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Habari za kijasusi za Marekani zinaonesha wapiganaji wa IS nchini Libya huenda waliongezeka mara dufu Libya miezi 12 hadi 18 iliyopita kutoka 4,000 hadi 6,000, kamanda mkuu wa Marekani anayesimamia Afrika Jenerali David Rodriguez, alisema wiki iliyopita.

Akihojiwa na Fox News, Bw Obama alisema operesheni ya vikosi vya Nato mwaka 2011 nchini Libya hata hivyo ilifaa.

Wakati huo, Libya ilikuwa imekabiliwa na maasi dhidi ya

Gaddafi aliyekuwa ameongoza kwa karibu miaka 41.