Mfalme akataliwa na watu wake visiwa vya Ufaransa

Futuna Haki miliki ya picha AFP
Image caption Visiwa vya Wallis na Futuna hupatikana kati ya Samoa na Fiji

Raia wengi wamezingira kasri la kifalme katika visiwa vinavyomilikiwa na Ufaransa vya Wallis na Futuna.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la utangazaji la visiwa hivyo.

Waandamanaji hao wanajaribu kuzuia kutawazwa kwa Mfalme mpya hapo Jumamosi.

Wiki iliyopita machifu wa kijadi walimteuwa Tominiko Halagahu, wa miaka 57 kama Mfalme.

Hata hivyo baadhi ya wanafamilia kwenye Ufalme wamepinga uteuzi huo na kusema lilikua jukumu lao kumchagua Mfalme.

Visiwa vya Wallis na Futuna vinapatikana kusini mwa Bahari ya Pasifiki kati ya visiwa vya Samoa na Fiji. Mwaka wa 1961 visiwa hivyo viliwekwa kama himaya ya Ufaransa.

Kuna Falme tatu kwenye visiwa hivyo na huwa na ushawishi katika masuala ya kisiasa.

Tayari falme mbili zimeteuwa Wafalme wao. Ufalme haoa haurithiwi, lakini hupewa watu waliochaguliwa na kundi kutoka kwa familia za kifalme.

Majadiliano ya nani awe Mfalme huchukua miezi hata miaka. Ufaransa ambayo husimamia visiwa hivyo inasema haitaingia kati, japo wanajeshi wamewekwa tayari katika kisiwa cha karibu cha Caledonia.