Raga: Kenya yashinda kombe la IRB Singapore

Haki miliki ya picha IRB
Image caption Raga: Kenya yashinda kombe la IRB Singapore

Kenya imeandikisha historia kwa kushinda mkondo wa Singapore wa ligi ya raga ya wachezaji saba kila upande duniani IRB .

Vijana wa kocha Benjamin Ayimba waliandikisha historia hiyo kwa kuichapa Fiji alama 30 kwa 7 katika fainali iliyokuwa ikitazamiwa na wengi.

Alama za Kenya zilifungwa na Samuel Oliech kisha nahodha na mfungaji try nambari mbili duniani Collins Injera akafanya mambo kuwa 10-0.

Oscar Ayodi Nelson Oyoo na kisha Frank Wanyama akaihakikishia Shujaa kombe lake kuu la kwanza katika ligi ya raga ya kimataifa ya IRB.

Kenya imeshiriki katika mashindano 114 ikitafuta ushindi huu.

Image caption Kenya imeshiriki katika mashindano 114 ikitafuta ushindi huu.

Sadfa ni kuwa japo timu hiyo ndiyo timu ya pekee katika msururu huo wa IRB inayosheheni wachezaji wasio wa kulipwa ilijifurukuta na kuilaza mabingwa watetezi na vinara wa ligi hiyo ya IRB Fiji .

Kenya ambayo inaorodheshwa katika nafasi ya 8 duniani sasa imejizolea alama 22 na kuipiku Uingereza kutoka nafasi ya 7 na alama 85.

'Shujaa' Kenya inavyojulikana ilianza kuonesha dalili za ufanisi mapema katika msururu huo wa Singapore ilipoilaza Argentina 15-12 ,katika hatua ya nusu fainali.

Hiyo ndiyo iliyokuwa mara kwanza kwa Kenya kufuzu nusu fainali tangu mwaka wa 2013.