Rais Kenyatta apongeza timu ya Kenya

Image caption Rais Kenyatta apongeza timu ya Kenya ya raga

Rais Uhuru Kenyatta ameipongeza timu ya Kenya iliyoweka historia kwa kushinda mkondo wa 8 wa ligi ya raga ya wachezaji saba duniani IRB huko Singapore.

Kupitia mtandao wake wa Twitter rais Kenyatta amesema kuwa anajiunga na wakenya milioni 40 wanasherehekea ushindi huo wa kihistoria.

''Jiunge nami kuwapongeza timu ya taifa ya raga ya wachezaji 7 kila upande kwa kuitwanga Fiji 30-7 katika fainali ya kombe la Singapore.''

''Kenya7s mumetupa kitu cha kujivunia''

Kenya yashinda kombe la raga la IRB Singapore

''Bidii na juhudi za Shujaa zimeiwezesha Kenya kuibuka mabingwa wa Singapore''

Msemaji wa rais bwana Manoah Esipisu amesema kuwa rais Kenyatta atawapokea wachezaji wa timu hiyo watakaporejea nyumbani.

Bw Esipisu anasewma kuwa rais Kenyatta aliwapigia simu mabingwa hao wapya kuwapongeza punde tu baada ya ushindi huo.

Vijana wa kocha Benjamin Ayimba waliandikisha historia hiyo kwa kuichapa Fiji alama 30 kwa 7 katika fainali iliyokuwa ikitazamiwa na wengi.

Image caption Collins Injera ndiye anayeorosheshwa wa pili bora katika ufungaji katika historia ya IRB

Kenya imeshiriki katika mashindano 114 ikitafuta ushindi huu.

Sadfa ni kuwa japo timu hiyo ndiyo timu ya pekee katika msururu huo wa IRB inayosheheni wachezaji wasio wa kulipwa ilijifurukuta na kuilaza mabingwa watetezi na vinara wa ligi hiyo ya IRB Fiji .

Kufuatia Ushindi huo wa kihistoria Kenya inaorodheshwa katika nafasi ya 7 duniani ikiwa na alama 85.