Hospitali ya Kenya kuwatibu bure wagonjwa wa Uganda

Image caption Mashine ya kutibu ugonjwa wa saratani ilioharibika

Hospitali moja nchini Kenya imeahidi kuwalipia matibabu wagonjwa wa saratani kutoka nchini Uganda kufuatia kuharibika kwa mashine inayotibu ugonjwa huo nchini Uganda.

Hospitali ya chuo kikuu Aga Khan imesema katika taarifa kwamba inaweza kutibu idadi ndogo ya wale wanaohitaji uuguzi.

Serikali ya Uganda tayari ilikuwa imetangaza kuwa itawasafirisha wagonjwa hao kupata matibabu nchini Kenya.

Kuharibika kwa mashine hiyo nchini Uganda kumewawacha maelfu ya wagonjwa katika hatari ya kukosa tiba.

Serikali ya Uganda imesema kuwa itagharamikia nauli ya usafiri pamoja na gharama nyengine kwa wagonjwa 400 wanaoelekea katika hospitali hiyo ya Nairobi.

Hospitali hiyo ya kibinafasi ina vitengo viwili vya kutibu saratani pamoja na madaktari sita wanaotibu ugonjwa huo

Tiba ya saratani inaweza kuwa ghali na wagonjwa wengi nchini Uganda haawezi kulipia matibabu yake.