Machar afuta mpango wa kurejea Juba

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Riek Machar

Serikali ya Sudan Kusini imesema kuwa kiongozi wa waasi Riek Machar, amefutilia mbali mpango wake wa kurejea Juba kwa muda usiojulikana.

Msemaji wa serikali Michael Makuei amesema kuwa makamu wa bwana Machar, alitaka kurejea Juba na silaha nzito nzito, zikiwemo, magari ya kivita, makombora na bunduki nzito nzito.

Aidha amesema kuwa serikali ya nchi hiyo tayari imeruhusu wanajeshi elfu moja mia tatu na sabini kati ya elfu moja mia nne na kumi kurejea Juba kuja kumlinda Bwana Machar.

Amesema kuwa utawala wa nchi hiyo hautaruhsu wanajeshi zaidi kurejeshwa Juba, kutokana na sababu za kiusalama.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Salva Kiir na Kiongozi wa waasi Riek Machar

Machar alitarajiwa kurejea nchini Sudan Kusini tangu hiyo jana kuchukua wadhifa wake wa zamani wa makamu wa kwanza wa rais.

Kiongozi huyo alitoroka Juba mwaka wa 2013 baada ya rais wa nchi hiyo Salva Kirr kumtuhumu kuongoza jaribio la mapinduzi ya serikali.