Kenyatta aidhinisha sheria iliyotakiwa na Wada

Kenya Haki miliki ya picha PSCU Kenya
Image caption Kenya ilikuwa imepewa hadi 2 Mei kuidhinisha sheria hiyo

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameidhinisha mswada muhimu wa kukabiliana na matumizi ya dawa za kutitimua misuli kuwa sheria.

Kuidhinishwa kwa mswada huo kunaondoa hatari ya Kenya kufungiwa kushiriki mashindano ya riadha ya kimataifa.

“Nataka ieleweke wazi kwamba hatua yangu kuidhinisha mswada huu kuwa sheria ni mwendelezo, na si mwisho, wa juhudi zetu katika kukabiliana na udanganyifu na ufisadi katika michezo na riadha,” amesema Rais Kenyatta baada ya kuidhinisha sheria hiyo.

“Nina imani na uwezo wa wanariadha wetu na naamini kwa dhati kwamba hatuhitaji kutumia njia za mkato ndipo tushinde.”

Ni moja ya masharti yaliyokuwa yamewekwa na shirika la kukabiliana na dawa za kuongeza nguvu mwilini katika riadha (Wada).

Shirika hilo lilikuwa limeipa Kenya makataa ya hadi tarehe 5 Aprili kuidhinisha sheria hiyo lakini baadaye muda ukaongezwa hadi 2 Mei.

Wada ilikuwa imesema juhudi za awali za Kenya hazikuwa zimetimiza viwango vinavyohitajika kimataifa.

Wanariadha kadha wa Kenya wamepigwa marufuku miaka ya karibuni baada ya kupatikana na makosa ya kutumia dawa hizo zilizoharamishwa.

Rais Kenyatta ameeleza matumaini kwamba wanariadha wa Kenya watafana katika Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Rio de Janeiro nchini Brazil Agosti mwaka huu.