Wapinzani wa Trump waungana kumzuia

Cruz Haki miliki ya picha AP
Image caption Cruz na Kasich wanataka kumzuia Trump kushinda majimbo zaidi

Wapinzani wawili wakuu wa Donald Trump katika kinyang’anyiro cha kumteua mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani wametangaza mipango ya kuungana kukabiliana na mgombea huyo.

Ted Cruz na John Kasich wanataka kushirikiana kupunguza uwezekano wa mfanyabiashara huyo tajiri kutoka New York kushinda mchujo katika majimbo zaidi.

Cruz, ambaye ni seneta wa jimbo la Texas, amesema atapunguza kampeni zake katika majimbo ya Oregon na New Mexico.

Kwa upande wake John Kasich, ambaye ni gavana wa Ohio, naye amesema atamwachia Cruz katika mchujo ujao jimbo la Indiana.

Bw Trump ameshinda majimbo mengi kufikia sasa, lakini bado hajapata wajumbe wanaohitajika kumpa ushindi wa moja kwa moja kabla ya Kongamano Kuu la Kitaifa la Chama mwezi Julai.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bw Trump amekuwa akisema viongozi wa chama hawataki ashinde

Amekuwa akilalamika mara kwa mara dhidi ya vigogo wa chama ambao amekuwa akidai wanapanga njama ya kumzuia kushinda uteuzi wa chama hicho.

Wapinzani wake wanasema iwapo Trump ataidhinishwa kuwa mgombea wa Republican basi chama hicho hakitaweza kushinda uchaguzi mkuu mwezi Novemba dhidi ya chama cha Democratic.