Muhtasari: Habari kuu leo Jumanne

1. Ukraine yakumbuka mkasa wa Chernobyl

Chernobyl Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu 30 walifariki papo hapo na wengine 4,000 wanaaminika kufariki baadaye

Ukraine leo inaadhimisha miaka 30 tangu kutokea kwa mkasa wa Chernobyl, ajali mbaya zaidi ya nyuklia kuwahi kutokea duniani. Ving’ora vitapigwa katika muda halisi ambao mlipuko ulitokea katika kinu cha nyuklia Aprili mwaka 1986. Paa lililipuka na moshi mkubwa wa vitu vyenye miale nururishi vikatapakaa kila mahali, na kusambaa kote katika mipaka ya Ukraine, hadi nchi jirani ya Belarus, na kote kaskazini mwa bara Ulaya.

2. Trudeau asikitishwa na kuuawa kwa mateka

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ridsdel alitekwa nyara miezi sita iliyopita

Waziri mkuu wa Canada, Justin Trudeau, ameelezea masikitiko yake baada ya mauaji ya John Ridsdel, mateka mmoja raia wa Canada ambaye alitekwa nyara na wapiganaji wa Kiislamu nchini Ufilipino miezi sita iliyopita.

Ameelezea kitendo hicho kama kisa cha mauaji baridi.

3. Polisi na wanajeshi wazima maandamano Misri

Haki miliki ya picha epa
Image caption Waandamanaji walikuwa wakipinga hatua ya serikali kukabidhi Saudi Arabia visiwa viwili

Operesheni kali ya maafisa wa polisi na wanajeshi nchini Misri, zilizima juhudi za waandamanaji waliojaribu kufanya mgomo wa kuipinga serikali ya taifa hilo katika mji mkuu Cairo.

Waandamanaji hao walikuwa wamekasirishwa na uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kurejesha visiwa viwili vilivyoko ndani ya bahari ya Sham chini ya udhibiti wa Saudi Arabia.

4. Mahakama yakataa marekebisho ya katiba Venezuela

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wapinzani walitaka muhula wa rais upunguzwe hadi miaka minne

Mahakama ya juu nchini Venezuela imekatalia mbali juhudi za mapendekezo ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo, kama ilivyopendekezwa na wanasiasa wa upinzani, ambao wana nia ya kupunguza muhula wa utawala wa Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro kutoka miaka sita hadi minne.

Upinzani unasema kuwa, taifa la Venezuela liko katika mgogoro kwa sababu ya miaka mingi ya mfumo wa utawala wa mrengo wa kushoto.

5. Maelfu waandamana North Carolina kuhusu jinsia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kunao wanaotaka Sheria ya Bunge Namba 2 (HB2) ifanyiwe marekebisho

Maelfu ya waandamanaji wamesafirishwa kwa mabasi hadi katika mji mkuu wa jimbo la North Carolina nchini Marekani ili kuunga mkono na wengine kupinga sheria mpya ya kitaifa ambayo inawapa masharti makali, watu wa mapenzi ya jinsia moja.

Sheria hiyo inasema kuwa watu wanatakiwa kutumia vyoo vya umma, ambavyo vinasahibiana na hali yao ya kijinsia ya kuzaliwa, sawa na inavyoorodheshwa katika cheti cha kuzaliwa, badala ya namna wanavyojitambua kijinsia.

6. Wakati bora wa kupewa chanjo ya homa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanasayansi wanasema chanjo hufanya vyema zaidi asubuhi

Na utafiti nchini Uingereza unaonesha kuwa, chanjo ya homa ni bora zaidi iwapo mtu atapewa majira ya asubuhi badala ya alasiri.

Watafiti wamebaini kuwa uwezo wa mwili wa mtu una nguvu mno kuwa na matoke bora iwapo mtu apata chanjo hiyo kabla ya saa tano mchana.