Watanzania waadhimisha Siku ya Muungano bila sherehe

Magufuli
Image caption Magufuli aliagiza pesa za sherehe zitumiwe kukarabati barabara Mwanza

Watanzania wameadhimisha Siku ya Muungano bila sherehe, baadhi wakiamua kutumia sikukuu hiyo kufanya usafi.

Rais wa Tanzania John Magufuli aliahirisha sherehe na badala yake akawataka Watanzania waiadhimishe wakiwa majumbani au wakiwa katika shughuli zao binafsi.

Siku hiyo hata hivyo bado ilisalia kuwa ya mapumziko kama kawaida.

Mwandishi wa BBC Esther Namuhisa alitembelea Uwanja wa Taifa unaotumika ambao kawaida hutumika katika sherehe za taifa.

Uwanja huo umefungwa na hakuna shamrashamra zozote zinazoendelea.

Katika eneo la Temeke, karibu na uwanja huo wa taifa, aliwakuta vijana wakifanya usafi.

Image caption Vijana katika eneo la Temeke wamekuwa wakifanya usafi

Siku ya Muungano huadhimishwa tarehe 26 Aprili kila mwaka kukumbuka siku sawa na hiyo mwaka 1964 ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja).

Dkt Magufuli alisema fedha ambazo zilipangwa kutumika kwa ajili ya kugharimia vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku zitumike kupanua barabara ya Mwanza Airport katika eneo linaloanzia Ghana Quarters hadi uwanja wa ndege wa Mwanza.

Image caption Sherehe zingegharimu karibu bilioni mbili za Tanzania

Inakadiriwa kwamba sherehe zingegharimu takriban shilingi bilioni mbili za Tanzania sawa na dola milioni moja za Kimarekani.

Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi kutatua msongamano wa mkubwa wa magari ambayo umekuwa ukiathiri shughuli eneo hilo.