Muhtasari: Habari kuu leo Jumatano

1. Trump asema anajihisi kama mgombea mteule

Trump Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Trump amesema hatabadilisha msimamo wake wa kisera

Nchini Marekani, tajiri Donald Trump amesema kuwa anajihisi sasa kama mgombea mteule wa urais wa chama cha Republican.

Alisema hayo alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake baada ya vyombo vya habari kutangaza kuwa amepata ushindi katika majimbo yote matano kaskazini mashariki mwa Marekani.

Majimbo hayo ni Connecticut, Delaware, Maryland, Pennsylvania na Rhode Island.

Katika shughuli za upigaji kura wa mchujo katika maeneo hayo, mtafuta nafasi katika chama cha Democratic Bi Hillary Clinton alimpiku muwaniaji mwenzake Bernie Sanders, ambaye alishinda katika jimbo moja tu la Rhode Island.

2. Watumishi wa umma kufanya kazi siku mbili kwa wiki

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Venezuela inakabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme

Serikali ya Venezuela imebuni mikakati ambayo itapelekea wafanyikazi wapatao milioni mbili wa serikali, kufanya kazi kwa siku mbili pekee kwa wiki katika kipindi cha majuma mawili.

Hatua hii inalenga kusaidia kukabiliana na uhaba wa umeme ambao unayumbayumba nchini humo.

Wafanyikazi hao wa umma na wale wanaofanya kazi katika sekta zinazomilikiwa na serikali watafika kazini siku za Jumatatu na Jumanne pekee hadi matatizo hayo ya nguvu za umeme yatakapodhibitiwa.

3. Mauzo ya Apple yashuka duniani

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mauzo ya simu za iPhone yameshuka sana

Kampuni kubwa mno ya teknolojia nchini Marekani - Apple, kwa mara ya kwanza kabisa tangu mwaka 2003, imeshuhudia kushuka kwa mapato yake katika robo ya kwanza ya mwaka.

Mauzo yake yalishuka kwa zaidi ya robo nchini China, soko lake kuu baada ya Marekani.

Aidha kumeshuhudiwa kushuka pakubwa kwa mauzo ya bidhaa ya Apple ya iPhone kote duniani.

4. Kiongozi mpya wa Tibet kutangazwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Serikali ya Tibet huishi uhamishoni India

Serikali ya Tibet iliyoko uhamishoni nchini India itatangaza hadharani leo nani ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha kumtafuta kiongozi wa kisiasa wa eneo hilo.

Kiti hicho kilibuniwa mnamo mwaka 2011, pale Dalai Lama alipojiuzulu kutoka kwa majukumu ya kisiasa.

Kiongozi wa sasa ni Lobsang Sangay, ambaye anatarajiwa na wengi kupata ushindi kwa muhula wa pili.

5. Uhispania kufanya uchaguzi

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mfalme wa Uhispania amesema uhasama wa kisiasa umeendelea

Uhispania inajiandaa kwa uchaguzi mwingine mkuu mwezi Juni mwaka huu, baada ya juhudi zake za kuunda serikali mpya kusambaratika.

Katika juhudi za siku mbili za mazungumzo, na viongozi wa chama tawala, mfalme wa Uhispania alisema bayana kuwa uadui wa kisiasa hauonekani kukoma hivi karibuni.

6. Korea Kaskazini kuandaa mkutano wa chama tawala

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Utakuwa mkutano wa kwanza chini ya Kim Jong Un

Na Korea Kaskazini imetangaza kuwa chama tawala cha kisiasa cha muda mrefu cha Wafanyikazi, kitaandaa mkutano wake kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 40, mwezi ujao mjini Pyongyang.

Ni mkutano wa kwanza chini ya kiongozi wa sasa Kim Jong Un. Mkutano huo wa kikomunisti utafanyika mjini Pyongyang mnamo Mei sita. Utaangaziwa pakubwa na viongozi wa kigeni kwani huenda swala muhimu likatangazwa.