Mazungumzo ya amani ya Burundi yaahirishwa

Burundi Haki miliki ya picha GETTY
Image caption Visa vya watu kuuawa vimeendelea kuripotiwa Burundi

Mazungumzo ya amani kuhusu mzozo wa kisiasa Burundi, ambayo yalipangiwa kufanyika wiki ijayo mjini Arusha, yameahirishwa.

Mashauriano hayo yalikuwa yamepangiwa kufanyika kuanzia tarehe 2 hadi 6 Mei chini ya mfanikishi aliyeteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa.

Taarifa kutoka afisi ya Bw Mkapa imesema mazungumzo hayo yameahirishwa kutoa nafasi kwa mashauriano zaidi na wadau.

“Inakadiriwa kwamba mazungumzo haya yatafanyika katika wiki ya tatu ya mwezi Mei,” taarifa hiyo imesema.

Awali, Bw Mkapa alikuwa ameeleza matumaini kwamba pande zote zingeshiriki.

Lakini siku chache baadaye upande wa serikali nchini Burundi ulilalamika kwamba haukuwa umepokea mwaliko rasmi.

Siku moja baadaye, serikali hiyo ilidokeza kwamba ingeshiriki.

Tulifikaje hapa?

  • Aprili 2015: Ghasia zazuka baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza atawania urais kwa muhula wa tatu.
  • Mei 2015: Mahakama ya Kikatiba yaunga mkono hatua ya Nkurunziza kuwania. Maelfu ya raia watoroka huku maandamano yakiendelea.
  • Mei 2015: Maafisa kadha wa jeshi wafanya jaribio la kupindua serikali. Jaribio lafeli.
  • Julai 2015: Uchaguzi wafanyika, na Bw Nkurunziza kutangazwa mshindi. Upinzani wapinga matokeo huku kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa akisema uchaguzi huo ulikuwa “mzaha”.
  • Desemba 2015: Watu 87 wauawa baada ya wanajeshi kujibu mashambulio yaliyotekelezwa katika vituo vya jeshi Bujumbura
  • Januari 2016: Madai ya kuwepo kwa makaburi ya pamoja yaibuka. Maafisa wa usalama wa Burundi watuhumiwa kutekeleza ubakaji wakikabiliana na wapinzani.
  • Aprili 2016: Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi lasema wakimbizi 250, 000 wametoroka Burundi na kukimbilia nchi jirani.
  • Aprili 2016: ICC yaanzisha uchunguzi wa awali kuhusu mauaji, dhuluma, ubakaji na kutoweka kwa watu Burundi.