Viongozi kujadili uhifadhi wa ndovu Afrika

Kenya Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kenya itateketeza shehena yake ya ndovu Jumamosi

Viongozi watatu wa nchi za Afrika wanakutana leo nchini Kenya kujadili njia za kuokoa ndovu ambao wanakabiliwa na tishio la kuangamia kutokana na ujangili.

Mkutano huo wa kwanza wa viongozi na watu mashuhuri duniani ambao unajulikana kama mkutano wa Giants Club utaongozwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Mkutano huo pia utawashirikishia viongozi wa makundi ya uhifadhi wa wanyama, wafanyabiashara na wanasayansi.

Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, Rais Kenyatta amesema ametoa wito kwa hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya biashara haramu ya pembe.

Rais Kenyatta amesema kuwa ndovu wanakabiliwa na hatari ya kuangamizwa na kizazi kipya cha wawindaji haramu, waliojihami vilivo na walio na uhusiano wa kimataifa, na matokeo yake yamekuwa mabaya sana.

Wataalamu wanasema idadi ya ndovu Afrika ilishuka kwa asilimia 90 karne iliyopita na wanaonya kuwa huenda wanyama hao wakaangamia katika miongo kadha ijayo.

Miongoni mwa wanaotarajiwa kuhudhuria kongamano hilo ni Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais wa Gabon Ali Bongo.

Baada ya mkutano huo, Kenya itateketeza shehena yake yote ya pembe, zenye uzani wa tani 105 ambazo ni sawa na pembe kutoka kwa ndovu 6,700.

Pembe hizo tayari zimepangwa katika eneo litakalotumiwa kuziteketeza katika mbuga ya taifa ya wanyama ya Nairobi.

Image caption Ndovu zaidi ya 30,000 huuawa Afrika kila mwaka

Shughuli ya kuzichoma itafanyika Jumamosi na itakuwa ndiyo idadi kubwa zaidi ya pembe kuchomwa kwa wakati mmoja duniani.

Kutakuwa pia na pembe vifaru za uzani wa tani 1.35.

Inakadiriwa kwamba pembe za ndovu zitakazoteketezwa zina thamani ya zaidi ya $100 milioni (£70m), na za vifaru $80 milioni (£55m).

"Hatuamini kwamba pembe zina thamani yoyote, (isipokuwa zikiwa kwenye wanyama walio hai) na tutaziteketeza pembe zote tunazohifadhi. Tutaudhihirishia ulimwengu kwamba pembe zina thamani tu zikiwa zikiwa kwenye ndovu wenyewe,” alisema Kitili Mbathi, mkurugenzi mkuu wa shirika la huduma za wanyamapori Kenya (KWS).

Afrika huwa na ndovu kati ya 450,000 na 500,000, lakini zaidi ya 30,000 huuawa kila mwaka na majangili wanaotafuta pembe.