Marekani yaitaka Urusi kushinikiza Syria

Haki miliki ya picha AFP

Marekani imeitaka Urusi kuishinikiza Syria kusitisha kuvamia raia na badala yake kuzingatia makubaliano ya kusitisha mapigano.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ametoa kauli hiyo baada ya hospitali moja iliyopo kwenye eneo la waasi kushambuliwa kwa ndege huko mjini Allepo, ambapo madaktari na watoto wameuawa.

Amesema Marekani imeshtushwa na shambulizi hilo ambalo limefanywa kwa kukusudiwa.

Zaidi ya watu sitini wameuawa mjini Aleppo lakini kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita katika maeneo yanayohodhiwa na serikali pamoja na waasi.

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema hali ni ya kusikitisha.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Josh Earnest amezungumzia kuongezeka kwa vurugu hizo.

'' Tunalaani vikali wimbo jipya la mashambulizi ya anga ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu sitini katika mji wa Aleppo katika kipindi cha saa ishirini na nne pekee.

Tumeshangazwa zaidi na shambulizi la anga lilipofanywa katika hospitali iliyopo mjini Aleppo ambalo limeuwa takriban wagonjwa kumi na nne na madaktari watatu- akiwemo pamoja na daktari pekee wa watoto katika mji huo''.

Maeneo ya mji wa Aleppo yamekabiliwa na mashambulizi mapya kutoka serikalini.

Wanaharakati wametoa picha za video zinazoonyesha waokoaji wanavyotafuta watu waliosalimika katika tukio hilo.