Wengi wajitokeza mazishi ya Papa Wemba

Papa
Image caption Watu wengi wamejitokeza katika kanisa la Notre Dame

Ibada ya mazishi ya mwanamuziki mashuhuri kutoka Janhuri ya Kidemokrasia ya Congo Papa Wemba inaandaliwa katika mji mkuu Kinshasa.

Mwili wa mwanamuziki huo utazikwa baadaye leo.

Nguli huyo wa nyimbo za rumba alifariki baada ya kuzirai akitumbuiza mjini Abidjan, Ivory Coast tarehe 24 Aprili.

Mwandishi wa BBC Poly Muzalia anasema mamia ya waombolezaji wamehudhuria ibada hiyo katika kanisa kuu la Notre Dame.

Gwiji huyo wa muziki wa lingala alizaliwa mnamo Juni 14 mwaka 1949, katika eneo la Lubefu, Wilaya ya Sankuru nchini DR Congo.

Jina lake halisi ni Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba.

Yeye alianza kazi ya muziki akiwa na umri mdogo mno ambapo alikuwa akimfuata mamake katika matanga na hivyo akaibukia kuwa mtunzi wa nyimbo za kuomboleza.

Vibao vyake ni kama vile Mwasi, Show me the way, Yolele, Mama, P na Rail On.