Aliyejaribu kuuza mtoto Afrika Kusini ahukumiwa

Haki miliki ya picha Gumtree

Mwanamke raia wa Afrika Kusini aliyejaribu kumuuza mtoto wake kupitia mtandao amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela ambacho kimeahirishwa.

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 20 alijaribu kuuza mtoto huyo wa umri wa miezi 19 rand 5,000 ($380; £250) kupitia soko la mtandaoni la Gumtree.

Wanaharakati wa kutetea haki za watoto wametofautiana kuhusu hukumu hiyo.

Baadhi wamefurahishwa na hatua ya mahakama kumuonea mwanamke huyo huruma lakini wengine wanasema mwanamke huyo alifaa kwenda jela kwa sababu ya vitendo vyake, tovuti ya IOL ya Afrika Kusini inasema.

Mwanamke huyo aliweka tangazo la kumuuza mvulana huyo baada ya mpenzi wake kugundua kwamba hakuwa babake mtoto huyo.

Mpenzi wake alimnyima usaidizi wa kifedha.

Haki miliki ya picha Gumtree
Image caption Mwanamke aliweka tangazo kwenye Gumtree

Mtoto huyo kwa sasa anasaidiwa na wahudumu wa kuwasaidia watoto.

Mwanamke huyo, ambaye jina lake haliwezi kutajwa kwa sababu za kisheria, alikamatwa baada ya polisi kujifanya wanunuzi.