Kim asifu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini

Kim Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kim amesifu mpango wa nyuklia wa taifa hilo

Mkutano mkubwa wa chama tawala nchini Korea Kaskazini umeanza huku Rais Kim Jong Un akisifu hatua zilizopigwa na taifa hilo katika kuunda silaha za nyuklia.

Mkutano huo wa chama cha Workers' Party ndio wa kwanza wa aina yake katika kipindi cha miaka 36.

Bw Kim amehutubia maelfu ya wajumbe, waliokusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Pyongyang.

Anatarajiwa kutia nguvu utawala wake wakati wa mkutano huo.

Wachanganuzi wa mambo wanatarajia pia kwamba atatangaza mpango kuhusu mageuzi ya kiuchumi huku akisisitiza azma ya taifa hilo ya kuendeleza silaha zake za nyuklia.

Kuna matarajio kwamba huenda jaribio la tano la bomu la nyuklia likafanyika wakati wa mkutano huo.

Wanahabari 100 kutoka nchi za nje wamealikwa kuangazia mkutano huo.

Haki miliki ya picha Reuters

Wanahabari hata hivyo wanafuatiliwa kwa karibu na maafisa wa serikali.

Hakuna mkutano mkuu wa chama uliofanyika wakati wa utawala wa babake Kim Jong-un, Kim Jong-il aliyefariki mwaka 2011.

Wakati wa mkutano wa mwaka 1980, uliofanyika kabla ya kuzaliwa kwa Kim Jong-un, ndipo Kim Jong-il alipotambulishwa kama mrithi wa mwanzilishi wa taifa hilo Kim Il-sung.

Licha ya kifo chake 1994, Kim Il-sung, aliyetawazwa kuwa “rais wa milele, kirasmi bado ndiye kiongozi wa mkutano huo mkuu wa chama ambao unatarajiwa kudumu siku kadha.