Dini hudhuru wanafunzi, wizara ya elimu China yasema

Dini Haki miliki ya picha Reuters
Image caption China hudhibiti sana shughuli za kidini

Serikali katika mkoa wa Gansu, China imeagiza wasimamizi wa shule kutekeleza kikamilifu marufuku ya kutokubalia shughuli zozote za kidini shuleni.

Wizara ya elimu katika mkoa huo uliopo kaskazini mashariki kwa nchi hiyo imechukua hatua hiyo baada ya msichana mmoja kuoneshwa kwenye video akikariri vifungu kadha vya Koran katika shule moja.

Shule hiyo imeshutumiwa vikali na maafisa hao wa wizara ya elimu.

Wizara hiyo kupitia taarifa imesema dini shuleni huathiri hali ya kiakili ya watoto.

Baadhi ya shughuli za kidini hukubaliwa nchini China lakini hudhibitiwa vikali.

Lakini waandishi wa BBC nchini humo wanasema serikali huwa makini sana kuhusu baadhi ya shughuli za kidini ambazo zinaweza kuathiri utambulisho wa kitamaduni wa Kichina.