Washukiwa wa mauaji Rwanda mahakamani Ufaransa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mauaji ya kimbari

Wakuu wawili wa zamani wa wilaya moja nchini Rwanda wamefikishwa mahakamani nchini Ufaransa kujibu tuhuma za kuhusika kwao katika mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.

Hii ni kesi ya pili inayohusiana na mauaji ya kimbari ya Rwanda inayosikilizwa na mahakama ya Ufaransa.

Rwanda imekuwa ikishutumu Ufaransa kuwa na nafasi katika mauaji ya kimbari na kutoshughulikia ipasavyo watuhumiwa wa mauaji ya kimbari waliokimbilia nchini humo.

Watuhumiwa hao ni Octavien Ngenzi mwenye umri wa miaka 58 na Tito Barahira aliye na umri wa miaka 64.

Mashitaka yanayowakabili ni kuhusika katika mauaji ya mamia ya watutsi waliokimbilia katika Parokia ya wilaya ya Kabarondo mashariki mwa Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari mwaka 1994.Wote wamekana mashitaka hayo.

Watuhumiwa hao walifuatana kuiongoza wilaya ya Kabarondo, karibu na mpaka na nchi ya Tanzania.

Bwana Octavien Ngenzi aliongoza wilaya hiyo kuanzia mwaka 1977 hadi 86 naye Tito Barahira akaongoza wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka 4 iliyofuatia.

Kulingana na mashahidi wa upande wa manusura wa mauaji hayo, watuhumiwa kama viongozi wa zamani wa wilaya hiyo,walikuwa na ushawishi mkubwa wa kuamuru mauaji yafanyike ama kuepusha yasitokee.

Mwaka 2009,watuhumiwa hao walihukumiwa kifungo cha maisha jela katika kesi iliyoendeshwa na mahakama za jadi maarufu Gacaca bila ya wao kuwepo.

Octavien Ngenzi alikamatwa mwaka 2010 katika kisiwa cha Mayottes huku mwenzie akikamatwa mjini Touluse miaka 2 baadae.

Image caption Mauaji ya Kimbari Rwanda

Hii ni kesi ya pili inayohusu mauaji ya kimbari ya Rwanda inayosikilizwa na mahakama ya Ufaransa.

Miaka miwili iliyopita mahakama ya Ufaransa ilimhukumu afisa wa jeshi la zamani la Rwanda Captain Pascal Simbikangwa kifungo cha miaka 25 jela kwa kumpata na hatia ya mauaji ya kimbari.

Wakili wake alipinga hukumu hiyo akiitaja kuwa ya kisiasa na kukata rufaa.

Rwanda imekuwa ikilaumu nchi ya Ufaransa kuwa na mwendo wa kujikongoja katika kuwashika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria watuhumiwa wa mauaji ya kimbari waliochukua fihadhi nchini Ufaransa.