Hollande azuru Jamhuri ya Afrika ya kati

Haki miliki ya picha Getty
Rais wa Ufaransa Francois Hollande anaizuri kwa mara ya tatu katika muda wa miaka minne Jamhuri ya Afrika ya kati - nchi iliyokuwa chini ya utawala wake enzi za ukoloni.

Ziara hiyo ambayo ni ya saa kadhaa inajiri wiki kadhaa baada ya rais wa CAR, Faustin Touadera, kuapishwa rasmi.

Uchaguzi wake unaonekana kama hatua muhimu kuelekea kurudisha amani na utulivu baada ya kushuhudiwa miaka kadhaa ya ghasia mbaya za kidini. Hatua ya kuamua kusitisha operesheni za jeshi la Ufaransa CAR kufikia mwisho wa mwaka huu huenda ikawa ndio mada kuu ya majadiliano.

Wasemaji wa rais anaarifu kuwa ziara hiyo inaashiria uwajibikaji wa Hollande kuunga mkono amani na utulivu katika taifa hilo.

Tangu 2013 kumeshuhudiwa mapigano kati ya waasi wa kiislamu Seleka na wanamgambo wa kikristo, anti-Balaka.

Kiongozi wa makundi ya kiraia Boniface Gonabana-Ndele ameiambia BBC kwamba suala la kupokonya wapiganaji silaha na kujumuishwa katika jamii makundi ya watu waliojihami ni lazima yajadiliwe wakati wa ziara ya Hollande.

Wengi katika mji mkuu, Bangui, wanatarajia pia kwamba kesi za unyanyasaji wa kingono unaowahusu wanajeshi wa Ufaransa pia litajadiliwa.